Na: Julieth Mkireri, MAIPAC KIBAHA
maipacarusha20@gmail.com
CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kimewafuturisha baadhi ya wadau wa michezo wakiwemo mashabiki wa Yanga na Simba pamoja na kufanya dua ya kuwaombea viongozi mbalimbali.
Dua hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF)Wallec Karia na rais wa CAF Dkt.Patrice Motsepe.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani Robert Munisi amesema kuwa wametumia siku hiyo kumuombea Rais Samia kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuiletea Nchi maendeleo sambamba na jitihada za kukuza michezo hapa nchini ukiwemo Mpira wa Miguu.
Lakini pia Munisi amesema dua hiyo imewagusa viongozi wa Mpira wa Miguu Tanzania na Afrika kwakuwa ndio viongozi bora na mfano kwa wengine katika kuendeleza soka na kuinua vipaji kwa vijana.
Munisi,mbali na hilo lakini pia imekuwa sehemu ya kusoma dua kwa ajili ya kuwakumbuka viongozi waliowatangulia akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa COREFA Imani Madega ambaye alifanya kazi nzuri katika mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani.
"Tunatambua mchango wa Rais Samia katika kuendeleza michezo hapa nchini sambamba na kuwakumbuka waasisi katika awamu zilizopita, yote hayo ni kuenzi michango ya waliotutangulia kupata sifa wanazostahili wakiwa hai na hata wakiwa hawapo tena duniani," amesema Munisi
Munisi, amesema kuwa mwaka huu ni mwaka wa kujifunza katika uandaaji wa futari na kusoma dua hiyo lakini COREFA utaweka utaratibu maalum wa kuhakikisha kila mwaka wanafuturisha na kuwaombea viongozi hao.
Mmoja wa walioshiriki katika futari hiyo Hamad Hassan ambaye ni Mjumbe kamati ya Utendaji kutoka Mkoa wa Kilimanjaro amepongeza COREFA kwa jambo hilo huku akisema wanastaili kuigwa.
Hassan,amesema kuwa tangu COREFA ilipoanzishwa miaka kadhaa iliyopita haikuwai kufanyika jambo la kufuturisha kama ambavyo uongozi uliopo ulivyofanya na kwamba ameutaka uongozi wa COREFA kuendelea na mpango huo muhimu kila mwaka .
Hassan ,amesema wanajifunza kutoka COREFA kuanzia tunzo wanazotoa, kuwa na ofisi na futari waliyoiandaa huku akiahidi kuendelea kujenga ushirikiano kati yao kuinua michezo hapa nchini.
Hatahivyo,katika hafla hiyo dua ya kuwaombea viongozi hao iliongozwa na shehe wa msikiti wa kwa Mathias Heri ambaye amesema kuwaombea viongozi ni jambo la kawaida ambalo kila mtu anapaswa kufanya hivyo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment