UTAFITI SUA WABAINI WANANCHI WANAOISHI VIJIJINI HAWALI MAYAI,HAWANYWI MAZIWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 27 March 2025

UTAFITI SUA WABAINI WANANCHI WANAOISHI VIJIJINI HAWALI MAYAI,HAWANYWI MAZIWA

 





Na Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha@gmail.com


MTAFITI kwenye mradi wa Kilimo,Chakula na Lishe (Food Land) kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA Profesa Suzan Nchimbi amesema Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu hicho umebaini kuwa wananchi wengi wanaoishi vijiji hawali mayai wala kunywa maziwa licha ya kufuga kuku, ng'ombe na mbuzi na hivyo wamekuwa wakikosa protini inayotokana na wanyama.


Profesa Nchimbi alitoa Matokeo ya utafiti wa mradi huo ambapo alizungumza na Waandishi wa Habari.


Alisema utafiti huo umefanyiwa katika Wilaya za Kilombero na Mvomero kwenye kijiji cha Kinda na ulifanywa kwa njia mbalimbali ikiwemo ya madodoso.


Profesa  Nchimbi alisema wakati wa utafiti huo walibaini kuwa wananchi hao wa vijijini wamekuwa wakifuga kuku wa mayai kwa dhumini la kibiashara ambapo mayai wamekuwa wakiuza na kupata fedha kwa ajili ya kutumia kwenye matumizi mengine.


"Pia kwenye unywaji wa maziwa wananchi tulichogundua wananchi hawanywi maziwa kwa sababu hawafugi ng'ombe na mbuzi wa maziwa,"alisema.


Alisema kuwa katika utafiti walioufanya katika kijiji cha Kinda walibaini kuwa wananchi wa kijiji hicho wanalima Kwa wingi maharage hivyo kupitia utafiti huo wameweza kuja na aina nne za mbegu za maharage ambazo zimeongezewa madini ya chuma na zinki.


Alitaja aina za mbegu  hizo maharage ni PIC 130, Nuha 629, Nuha 660 na Mashamba na tayari aina hizi zote zipo kwenye hatua mbalimbali za kufanyiwa majaribio kwenye Mamlaka mbalimbali ikiwemo TOSCI," amesema Prof. Nchimbi.


Profesa Nchimbi alisema utafiti ulilenga pia kwenye ufugaji wa samaki Kwa kuangalia chakula bora cha samaki wa kufungwa lakini pia namna bora ya kuhifadhi mazao hasa matunda mbalimbali yakiwemo maparachichi.


Awali akitoa taarifa ya utafiti huo mmoja wa washiriki wa utafiti huo Profesa Dismas Mwoseba alisema utafiti huo ilianza mwaka 2020 na unafanywa kwenye nchi sita ambazo ni Morocco, Tunisia, Ethiopia, Kenya, Uganda na Tanzania ambapo Kwa Tanzania utafiti huo umefanyika katika mkoa wa Morogoro wilaya ya Kilombero na Mvomero lakini pia katika mkoa wa Dar es Salaam.


Profesa Mwoseba alisema mradi huo umelenga kwenye masuala ya kilimo, elimu, afya na lishe ambapo kwenye upande wa elimu wamebaini kuwa vijana wengi wa kwenye kijiji cha Kinda hawajui kusoma hali ambayo inawafanya washindwe kusoma vipeperushi na majarida mbalimbali yanayoeleza masuala ya lishe na hivyo kujikuta wakishindwa kuzingatia masuala ya lishe.


Mwisho.



No comments: