Na Julieth Mkireri, MAIPAC MKURANGA
maipacarusha20@gmail.com
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ussi amewakumbusha Vijana kuendelea kutunza amani iliyopo hususani katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi Mkuu Octoba mwaka huu.
Ussi ametoa rai hiyo jana alipokuwa akizungumza baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea mradi wa uwezeshwaji Vijana kikundi cha Mwanambaya One bodaboda ambacho kilianzishwa kwa ajili ya kuwaunganisha vijana wenye dhamira moja ya kufanya kazi ya kusafirisha abiria na mizigo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa na kufanya ukaguzi wa kikundi hicho kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru amesema vijana wameonyesha matumizi mazuri ya fedha walizopata.
Amesema Mwenge wa Uhuru mwaka huu una ujumbe wa kushiriki uchaguzi kwa amani 'jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu' ambao Vijana wanatakiwa kuuzingatia.
Pia amewataka wananchi kutunza kadi zao za kupigia kura Ili waweze kushiriki uchaguzi Mkuu kwa mujibu wa Katiba.
Akisoma taarifa ya kikundi hicho mmoja wa wanakikundi Adam Kisigalile alisema kikundi hicho chenye lengo la kuwainua kiuchumi kwa mara ya kwanza kilipata mkopo wa sh. miln 12 .7 na kununua pikipiki nne na mwaka 2024 walipata mkopo wa sh Miln 60 kwa ajili ya Ununuzi wa gari yenye ukubwa wa tani mbili.
"Kupitia mikopo hii ya Halmashauri kikundi kimepata mafanikio kwa kuongeza pikipiki na wanachama kununua viwanja vya makazi na kuongeza mapato kutoka 700,000 hadi 1,700,000 kwa mwezi," amesema
Awali akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Kisarawe, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nasri alisema Mwenge huo utapitia miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh. Biln 97.
Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Mkuranga umezindua mradi mmoja, umeweka mawe ya Msingi na kukagua miradi mingine ya Maendeleo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment