Na: ASKOFU BAGONZA
1. Taifa hili bila CCM imara, litayumba sana. Sina hakika kama bado.
2. Ili CCM iwe imara inahitaji upinzani imara. Hatuna utamaduni imara wa kukosoana ndani ya chama kimoja na kubaki salama.
3. CCM dhaifu na upinzani dhaifu ni chanzo cha taifa lililojaa machawa, rushwa, uzembe, amani bila haki, ukandamizaji wa kila namna na uporaji wa raslimali za nchi.
4. Marais wetu wanatokana na vyama. Tusiwategemee sana kuwa “neutral” katika masuala ya kisiasa. Chini ya mfumo wa sasa, hata rais mlokole hawezi kusaidia. Hata JKN yalimshinda akatamka “siwezi kuwaachia mbwa taifa langu”!
5. Huu ni mwaka wa uchaguzi. Tamaa ya madaraka ndani ya CCM ni kama yote. Ubinafsi ndani ya upinzani ni kama wote. Nani mwathirika wa hali hii?
6. Mwathirika wa kwanza ni nchi/taifa. Tutakosa uwajibikaji (checks and balances) na hapo hata wanaotaka watawale peke yao wataumia. Miradi yote ya kimkakati itakosa ulinzi. Rais dikteta wa kuumiza chama chake na vingine ndiye atakayeshangiliwa kwa muda kabla ya majuto.
7. Mwathirika wa pili ni CCM. Itakosa chama na mfumo wa kuiwajibisha. Kitateka, kitaua, na baadaye kujiteka na kujiua. Ubinafsi wa wapinzani ni kuionea CCM kwa sababu uwezo wake wa kujidhibiti iliukabidhi kwa vyombo vya dola.
8. Mwathirika wa tatu ni mwananchi wa kawaida. Hivi wananchi hawana mahali pa kwenda kupata hata haki ya kusikilizwa. Viongozi wa kuchaguliwa wanafilisiwa na wananchi wenye matatizo ambayo yangetatuliwa na mifumo (karo, misiba, matibabu, ajira, dhamana, nk). Wabunge na madiwani wako hoi.
9. Kukosekana kwa uimara wa upinzani kumeifanya CCM na serikali kuua “ugatuzi” na kupeleka madaraka yote kitovuni Dodoma (Centralization). Hiki ni kichaka cha uzembe na mateso kwa wananchi. Mtu anaandika barua Dodoma, haijibiwi. Anafuatilia, anaambiwa rudi wilayani bila majibu! Mamwinyi walio Dodoma wanaamini kila mtanzania ana simu na kifurushi cha kutumia mtandao😭😭
10. Anayeshangilia kuzima taa zote na kuwasha moja si Mzalendo. Anayeshangilia upinzani kusambaratika si Mzalendo. Anayetumia fedha kuhairisha uwezekano wa kuwajibika na kuwajibishana si Mzalendo. Taifa letu ni kubwa kuliko chama chochote. Taifa kubwa namna hii lenye mtazamo mmoja; Nani analitaka na kwa manufaa ya nani?
11. Nampongeza Mtani wangu Mzee Wasira kwa kuanza kukemea rushwa za uchaguzi ndani ya CCM. Napongeza wanaojitolea kupatanisha wapinzani katikati ya kukejeliwa. Rushwa za uchaguzi zinalipokonya taifa na watu waadilifu lakini wasio na fedha. Migogoro ndani ya upinzani inawanyima wananchi utetezi na uwajibikaji wa watawala wetu.
Hekima ya Wajaluo:
“ Ngedere mchanga aliona msitu unateketea, akashangilia asijue usiku atalala wapi?”
No comments:
Post a Comment