DC KAGANDA AWAONGOZA VIONGOZI WA BABATI ZIARA YA MAFUNZO SERENGETI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 9 April 2025

DC KAGANDA AWAONGOZA VIONGOZI WA BABATI ZIARA YA MAFUNZO SERENGETI

 




Na Epifania Magingo,Manyara 


Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, ameongoza ziara ya kikazi katika Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara, akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wa Chama, kwa lengo la kujifunza kuhusu utekelezaji wa uzio wa umeme unaozunguka maeneo ya hifadhi na vijiji jirani.


Ziara hiyo imefanyika kufuatia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Babati kuhusu tembo na wanyama wengine wakali wanaoharibu mazao, kuleta hofu, na kuathiri shughuli za kiuchumi. 


Wananchi wameiomba Serikali kusaidia kujenga uzio wa umeme kama hatua ya kudumu ya kuondoa migongano kati yao na wanyamapori.


Katika maelezo yake, Kaganda amesema

ameamua kuja kujifunza kutoka Serengeti baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwepo wa uzio wa umeme kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Babati nao waishi kwa amani na wajikite kwenye kilimo bila hofu ya tembo au wanyama wakali.


Wananchi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Serengeti walieleza namna uzio huo ulivyobadili maisha yao, wakisema sasa wanaendelea na shughuli zao kwa utulivu bila uharibifu wa mazao au madhara kutoka kwa wanyama.


Kwa upande wake, Hassan Mtunzi Afisa Mahusiano na Mwanasheria wa Shirika la Ngurument Fund ambalo limeshirikiana na Serikali kuwezesha ujenzi wa uzio huo, alifafanua kuwa lengo la awali lilikuwa kuwalinda faru waliowekwa hifadhini, lakini baadaye imeonekana uzio huo ni suluhisho pana kwa wanyamapori wengine wanaosababisha madhara kwa binadamu.


"Uzio huu umekuwa mkombozi kwa wakulima,Siyo tu kwa faru, bali tembo na wanyama wengine wote wakali wanadhibitiwa bila kuumiza yeyote. Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa uhifadhi," alieleza Mtunzi.


Kaganda ameahidi kufikisha mafunzo hayo katika mamlaka husika na kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa ili kuwanusuru wakulima wa Babati, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kutatua kero za wananchi kwa vitendo.

No comments: