RUWASA YATATUA KERO YA MAJI KWALA. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 9 April 2025

RUWASA YATATUA KERO YA MAJI KWALA.

 





Na Julieth Mkireri, MAIPAC KIBAHA 


maipacarusha20@gmail.com 


MWENGE wa Uhuru umezindua mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya sh. Biln 1.494 ambao unakwenda kuhudumia wananchi 6,407 wa Vijiji vya Kwala na Mwembe ngozi. Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.


Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kibaha Mhandisi Debora Kanyika amesema mradi huo uliibuliwa na wananchi baada ya Changamoto ya kukosa huduma ya maji safi na salama kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyolengwa mwaka 1974.


Mhandisi Kanyika amesema kabla ya mradi huo wananchi walikuwa wakitumia maji yasiyokuwa safi  na salama ambayo yalikuwa yakiletwa na magari kwa gharama ya sh. 300 kwa ndoo ya lita 20.


"Baada ya kutekeleza miradi huu wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa gharama ya sh.40 kwa ndoo ya lita 20 kwa matumizi ya nyumbani na sh. 50 kwa matumizi ya viwandani na kwasasa mradi unaendeshwa na chombo cha utoaji wa huduma  ya maji ngazi ya Jamii Minazi mikinda," amesema.


Pia Meneja huyo amesema chanzo cha maji cha mradi huo ambao uko Kijiji cha Minazi Mikinda ni kisima chenye uwezo wa kutoa lita 43,000 kwa saa ambacho kina urefu wa mita 33.


Mhandisi Kanyika amesema mradi huo ambao mkataba wake ulisainiwa mwezi Machi mwaka 2022  na kukamilika April mwaka 2024 upo kwenye muda wa matazamoo hadi mwisho wa mwezi huu na kwamba wakati wa ujenzi wananchi 100 walipata Ajira za muda na sasa Ajira za kudumu 10 zimepatikana.


Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi akizindua mradi huo aliwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ya maji  Ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu.


Salma Mohamed na Zainab Hussein ni kati ya wakazi wa Minazimikinda ambao wameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo ambao umewapunguzia adha ya kutafuta maji mbali na makazi yao.


Salma amesema kwasasa wanaweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo.


Mwisho

No comments: