![]() |
Mwandishi Mkuu wa Sheria Onorius Njole |
![]() |
Wajumbe wa Kikosi kazi pamoja na sekretarieti kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria |
Na Lilian Kasenene, Mwanza
maipacarusha20@gamil.com
Katika kuhakikisha maamuzi na maazimio ya Serikali ya kutumia Lugha ya Kiswahili kwenye kuendesha kesi mahakamani na katika utoaji wa hukumu, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria tayari imemaliza kazi ya kutafsiri sheria kuu zote 446 za Tanzania kwa Lugha ya Kiswahili.
Hayo yamebainishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Onorius Njole wakati akizungumza na Kikosi kazi cha Wataalamu nguli wa Lugha ya Kiswahili na sheria nchini waliokutanishwa na Ofisi yake kwaajili ya kuandaa Muongozo wa Ufasili wa Sheria unaofanyika jijini Mwanza.
“Tanzania tuna sheria kuu zipatazo 446, na tunatambua sote kuwa sheria hizo zote zilikuwa zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza lakini baada ya maagizo ya Serikali ya kutaka mahakama kutumia lugha yetu Mama na sheria kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili tulifanya kazi hiyo kubwa na nzito lakini tunafurahi sasa kusema kuwa tumeikamilisha," alisema.
"Pia tuna rasimu ya sheria kuu zote kwa Kiswahili hivyo kupata muongozo huu wa ufasiri utatusaidia sasa kutumia kupitia rasimu hizo ili ziwe na mfanano pamoja na kuondoa mkanganyiko kabla ya kuanza kutumika,” alieleza Njole.
Aidha Njole alisema kuwa baada ya kumaliza zoezi la urekebu wa sheria toleo la mwaka 2023 na kufanya ufasili wa sheria hizo wameona itakuwa na maana kubwa kama wataweza sasa kutoa toleo la sheria hizo zote zilizorekebiwa kwa lugha ya Kiswahili kwa kufuata muongozo rasmi ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao wa fedha ili ziweze kuanza kutumika.
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria nchini alisema huko nyuma wamekuwa wakifanya ufasili wa sheria kawaida bila kuwa na chombo maalumu cha kuwaongoza kuhakikisha kunakuwa na mfanano lakini wanaamini baada ya kuwepo kwa Mwongozo huo sasa kutawezesha kuandika vizuri sheria kwa Kiswahili na kufasili vyema zilizopo.
“Kwa hiyo Mwongozo huu wa ufasili wa sheria tunauhitaji sana ili hata inapotokea changamoto kutokana na tafsiri hiyo tunarudi kwenye Mwongozo kama msingi wa ufasili kuliko hivi sasa ambapo kila mtu anafanya ufasili kwa kutumia utashi na uelewa wake hali inayoweza kuleta misuguano ya kisheria isiyo ya lazima na kupotosha maana ya dhana husika.
"Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Hayati Dk John Pombe Magufuli wakati akihutubia Bunge alisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi kwa kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili,"alisema.
Katika kutekeleza azma hiyo, Mwaka 2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Tafsiri za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti la kwamba lugha ya sheria sasa ni Kiswahili na lugha ya kutumika katika vyombo vya utoaji haki nchini nay oni Kiswahili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment