Mkurugenzi Mtendaji Tanesco afariki dunia kwa ajali - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 13 April 2025

Mkurugenzi Mtendaji Tanesco afariki dunia kwa ajali




NA MWANDISHI WETU, Mara


maipacarusha20@gmail.com 


MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga amefariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 katika ajali ya gari iliyotokea Bunda mkoani Mara.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amefafanua kuwa limetokea kati ya saa 6 hadi 7 usiku wa kuamkia leo (Aprili 13,2025.

"Ni kweli tukio lipo na amefariki dunia," amesema  Mtambi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema ni baada ya gari la Mkurugenzi lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Bunda kugongana na lori.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari lililokuwa limembeba Mkurugenzi aina ya Toyota Land Cruiser kumkwepa mwendesha baiskeli kisha kupoteza mwelekeo na kugongana na lori.

"Tukio limetokea Bunda saa 7.30 usiku baada ya dereva wa gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyombeba mkurugenzi kumkwepa mwendesha baiskeli na kugongana na lori kisha kupelekea vifo vya dereva na bosi wake," amesema Kamanda Lutumo

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mara, Nickson Babu amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH) huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu taratibu nyingine.

No comments: