FRANONE MINING YATOA MILIONI 10 KUJENGA UZIO NAISINYAI SEC - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 15 April 2025

FRANONE MINING YATOA MILIONI 10 KUJENGA UZIO NAISINYAI SEC

 



Na Mwandishi wetu, Simanjiro 


maipacarusha20@gmail.com 


KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Franone Mining LTD, inayochimba madini ya Tanzanite kitalu C na D, imejitolea shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule ya sekondari Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.


Mkuu wa shule ya sekondari Naisinyai, Mbayani Kivuyo akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha sita ya shule hiyo amesema wanaishukuru kampuni ya Franone Mining LTD kwa msaada huo.


Kivuyo amesema kukamilika kwa uzio huo kutanufaisha shule hiyo kwani ukosefu wake inakuwa ni changamoto kubwa kwa shule ya sekondari Naisinyai yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita.


"Ukosefu wa uzio wa shule ni changamoto kubwa kwetu kwani hakuna usalama wa kutosha kwa mali za shule na wanafunzi wanaosoma kwenye shule hii," amesema Kivuyo.


Amesema kampuni ya Franone Mining LTD, imekuwa chachu ya maendeleo kwao kwani wamekuwa msaada pindi wanapokuwa na uhitaji wa msaada.


Amesema kutokana na hali hiuo wanaikabidhi zawadi ya keki kampuni ya Franone Mining LTD, ili kuonyesha shukurani kwa kuwajali kwani hivi sasa wataendeleza ujenzi wa uzio wa shule yao.


"Tunashukuru sana kwa hili, salamu za asante ziwafikie wakurugenzi wote wa Franone Mining LTD, Onesmo Mbise na Francis Matunda na Meneja wa kampuni Vitus Ndakize," amesema Kivuyo.


Mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari Naisinyai, Simon Siria ameishukuru kampuni ya Franone Mining LTD, kwa msaada huo wa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa uzio.


Siria amewataka wanafunzi wa shule hiyo wanaotarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita, kuhakikisha wanafaulu vyema mitihani yao.


"Mnapaswa kutambua kuwa hapa mmekuja kufanya nini ili mwisho wa siku mpate mlichotarajia kukipata kupitia mitihani mtakayoifanya," amesema Siria.


MWISHO

No comments: