![]() |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango |
Na Anangisye Mwateba-Dodoma
maipacarusha20@gmail.com
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango leo amewaongoza mamia ya wananchi wa jiji la Dodoma kuadhimisha miaka 103 ya Kuzaliwa Mwalimu Mwalimu Julius Nyerere katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Maadhimisho haya huandaliwa na Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Katika hotuba yake Mhe. Mpango alisema kuwa kupitia Falsafa ya Mwalimu Nyerere ya Utunzaji wa Misitu na Uhifadhi wa Mazingira imefanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupongezwa kwa jitihada zake za kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhe. Mpango alisema kuwa Mhe. Rais, amekuwa mstari wa mbele na kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia hapa nchini, barani Afrika na Kimataifa.
“Mhe. Rais anaratibu utekelezaji wa Programu ya Nishati Safi ya Kupikia ya Bara la Afrika iliyozinduliwa mwaka 2023 na inayolenga kuwezesha wanawake kutumia nishati safi ya kupikia katika Bara la Afrika. Kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia tutapunguza uzalishaji wa gesijoto, uharibifu wa misitu na mazingira, kupunguza athari za kiafya, kiuchumi na kijamii zitokanazo na matumizi makubwa ya kuni na mkaa pia kuleta usawa wa kijinsia” Alisema Mhe. Mpango
Vilevile Mhe. Rais amekuwa akiweka jitihada za kuwahamasisha watanzania kupanda miti, kudhibiti taka kwa kufanya usafi wa mazingira na biashara ya kaboni.
Akimkaribisha Mhe. Mpango, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Dunstan Kitandula alisema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeshapata kiwanja katika eneo la Mtumba ndani ya Jiji hili la Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Makumbusho ya Marais.
Mhe Kitandula aliongeza kuwa Ndani ya Makumbusho hiyo, kutakuwa na sehemu itakayoonesha historia na mchango wa Mwalimu Nyerere kitaifa na kimataifa. Aidha, eneo la Kongwa ambalo linaonesha mchango wa Mwl. Nyerere na mkoa wa Dodoma katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, limetangazwa kwa Tangazo la Serikali Namba 166 la tarehe 15 Machi, 2024 kuwa Urithi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment