DC BAGAMOYO AWATAKA WATENDAJI KWENDA KWA WANANCHI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 10 May 2023

DC BAGAMOYO AWATAKA WATENDAJI KWENDA KWA WANANCHI


MKUU Wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi



 NA JULIETH MKIRERI, MAIPAC CHALINZE 



MKUU Wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi amewataka watendaji wa Halmashauri ya Chalinze kuhakikisha wanawafikia wananchi sambamba na kusimamia  kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kukaa ofisini.

Okashi ametoa maelekezo hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze ambapo alisema sio wakati sasa wa watendaji kukaa ofisi wakati wananchi wanawahitaji kuwatatulia kero zao.

Alisema kitendo cha baadhi ya watumishi kuendelea kukaa ofisini ni moja ya sababu zinazochangia kuzorota kwa utekelezaji wa maangizo ya viongozi wa juu.

“Tukumbuke Rais wetu Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali haitapendeza akisikia kuna jambo halisimamiwi vizuri, napenda tufanye kazi kwa ushirikiano tumsaidie Rais kama alivyotuamini” alisema.

Aidha aliwakumbusha Madiwani kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao na hiyo itasaidia kuwaelezea wananchi kuhusiana na utekelezaji wa ilani namna unavyofanyika.

Akizungumzia suala la ukatili wa kijinsia Okashi alisema, Viongozi wa Wilaya hiyo wanaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya Kata na watashuka hadi kwenye Vijiji  na baadae nyumba kwa nyumba ili wananchi waelewe namna ya kutokomeza ukatili.

“Rais wetu ameonyesha mfano na kila siku anasisitiza tutoe elimu kwa jamii, na sisi tutazungumza na wazazi na watoto tutatumia njia mbadala ambayo wataelewa kwa urahisi ili hata wale wanaofanyiwa vitendo hivi wasiwe waoga kutoa taarifa” alieleza Mkuu huyo wa Wilaya.

Kadhalika Okashi aliwataka Maofisa Ustawi wa Jamii kuachana na tabia ya kukaa ofisini badala yake waunge juhudi za Rais za mapambano ya kupinga ukatili  kwa kwenda kutoa elimu kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya kutokana na vitendo vya ukatili kuendelea kujitokeza kwenye maeneo mbalimbali ni vema Madiwani nao kwa nafasi zao wakashiriki kutoa elimu kwenye jamii.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassan Mwinyikondo akizungumza katika Baraza hilo alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira kuhakikisha wanawaelezea wananchi kuhusiana na utekelezaji wa agizo la Rais Samia la kuwasambazia maji wananchi .

Agizo hilo lilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassani aliposhiriki maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maji yaliyofanyika Mkoani Pwani mwaka 2022 ambapo aliahidi kuipatia DAWASA  sh. Milion 500  kwa ajili ya kazi ya usambazaji wa maji.

Katika sherehe hizo Rais pia a;iahidi kuongeza kiasi kingine cha fedha kama hiyo baada ya mrejesho wa mzuri wa matokeo ya fedha ya awali.

Mwingyikondo aliwataka watendaji kutokaa kimya kwa yale yanayofanywa na Serikali katika jamii kwani kwa kufanya hivyo wanasababisha wananchi wasijue miradi iliyotekelezwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

No comments: